Katika kuimarisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, STEPS Tanzania kupitia ufadhili wa Global Fund (C7) imetekeleza mbinu bunifu ya kuwashirikisha vijana wa bodaboda wanaojitolea kusambaza kondomu na kuhudumia vifaa vya kugawa kondomu (Condom Dispenser) katika jamii.
Mpango huu unatekelezwa katika mikoa ya Njombe, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mbeya, Songwe na Ruvuma. Baada ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi, bodaboda hawa husambaza kondomu katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama baa, nyumba za wageni, vilabu vya usiku, minada na sehemu nyingine za mikusanyiko ya kijamii.
Kutokana na uelewa wao wa mitaa na urahisi wa usafiri, wanafika kwa haraka hata katika maeneo yasiyofikika kirahisi na wahudumu wengine wa afya ya jamii. Kwa kushirikiana na wasimamizi wa VVU ngazi ya jamii, wanahakikisha:
· Kondomu zinawasilishwa kwa kuzingatia mpango uliopangwa.
· Vifaa vya kugawa kondomu vinajazwa upya kwa wakati.
· Taarifa za usambazaji na mahitaji zinawasilishwa kwa Mratibu wa UKIMWI ngazi ya jamii kwa ufuatiliaji.
Furaha kwa Wanufaika
Jamii imepokea kwa mtazamo chanya huduma hii. Wahudumu wa baa na wamiliki wa nyumba za wageni wanasema sasa hawapati tena changamoto ya kuishiwa na kondomu, hali inayoongeza uhakika wa upatikanaji wa kinga wakati wote.
“Kwa sasa tuna uhakika wa upatikanaji endelevu. Bodaboda wanapita mara kwa mara kukagua na kujaza,” anasema mmiliki wa nyumba ya wageni mkoani Mbeya.
Upatikanaji wa kondomu kwa wakati umeimarisha matumizi sahihi ya kinga na kuongeza mwitikio wa jamii katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.
Mchango kwa Malengo ya Mradi
Utekelezaji huu unaunga mkono malengo ya STEPS Tanzania chini ya ufadhili wa Global Fund, yakiwemo:
Kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa 85% (kutoka kiwango cha mwaka 2010) ifikapo 2025.
Kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa 80% kutoka kiwango cha mwaka 2010.
Kupunguza unyanyapaa unaohusiana na VVU hadi chini ya 5%
Kwa kuongeza upatikanaji wa kondomu na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji, bodaboda wanasaidia kuboresha takwimu za usambazaji, kutambua maeneo yenye mahitaji makubwa, na kupanga mikakati sahihi ya kinga.
Ubunifu Unaogusa Jamii
Ushirikishwaji wa bodaboda umeongeza ufanisi wa usambazaji na kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda afya yake. Kupitia mbinu hii, STEPS Tanzania inaonesha kuwa pale jamii inapowezeshwa na kuaminiwa, inakuwa sehemu ya suluhisho.
Leo, bodaboda si tu wasafirishaji wa abiria, bali ni washirika muhimu katika kulinda maisha na kujenga jamii yenye afya bora.
