STEPS Tanzania Yafikia Jamii Tanga Kupitia Mradi wa Momentum
STEPS Tanzania kupitia mradi wa Momentum, unaotekelezwa katika Mkoa wa Tanga, imefanikiwa kuendesha vikao vya kufikia jamii na kutoa elimu kuhusu athari za matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na mikakati ya kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya madawa ya kulevya (Harm Reduction), hususan kwa wanawake wanaoishi na/au wanaoathirika na matumizi ya madawa ya kulevya katika kata za Mwanzange na Chumbageni.

Vikao hivyo
viliongozwa na timu ya Waelimishaji Rika, kwa kushirikiana na Mental Health
Coordinator, pamoja na uongozi wa Kata (LGA). Ushirikiano huu uliwezesha kutoa
hamasa na elimu kwa wanajamii, kwa lengo la kujenga jamii iliyo salama, yenye
uelewa wa kutosha juu ya namna ya kuwahudumia na kuwaunga mkono watu
wanaoathirika na matumizi ya madawa ya kulevya bila unyanyapaa.
Akizungumza
katika vikao hivyo, Mental Health Coordinator alielezea kwa kina huduma
mbalimbali zinazotolewa katika Kliniki ya MAT (Medication Assisted Treatment),
na kusisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuendelea kuwapa ushirikiano watoto
wao walioanza matibabu ya MAT. Alisisitiza kuwa kuepuka unyanyapaa ni hatua
muhimu inayowasaidia wagonjwa kurejea katika hali bora ya afya ya akili na
ustawi wa maisha yao kwa ujumla.
Mbali na hilo,
wanajamii walipatiwa elimu juu ya:
Magonjwa ya
kuambukizwa kwa kuchangia sindano, yakiwemo VVU
Kifua Kikuu (TB)
miongoni mwa watu wanaotumia madawa ya kulevya
Afya ya uzazi na
uzazi wa mpango kwa wanawake wanaotumia madawa ya kulevya

Aidha, timu
ilitekeleza zoezi la kutembelea maeneo hatarishi (Hotspots) kupitia programu ya
Moonlight Outreach katika eneo la Sabasaba. Katika matembezi hayo ya usiku,
Waelimishaji Rika waliweza:
Kutoa elimu ya
VVU na UKIMWI, TB, na Harm Reduction
Kugawa kondomu
Kutoa hamasa kwa
waraibu waliokutwa maeneo hayo kufanya uchunguzi wa afya zao na kujiunga na
huduma stahiki
Jumla ya wanajamii 105 walihudhuria vikao vya elimu katika Kata ya Chumbageni na Mwenzange. Vilevile, waraibu waliokutwa wakati wa Moonlight Outreach walipewa fursa ya kujiunga na programu za uwezeshaji kiuchumi zinazotolewa na asasi washirika, zikiwemo MUKIKUTE, OYARB, na Gift of Hope. Kupitia Mfuko wa CHAC, huduma pia zinaendelea kuwafikia WAVIU ambao pia ni waraibu wa madawa ya kulevya.

STEPS Tanzania inatoa shukrani na pongezi za dhati kwa ViiV Healthcare pamoja na MUKIKUTE kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa programu za kupunguza madhara kwa wanawake wanaotumia madawa ya kulevya na wenza wao katika Mkoa wa Tanga.
Picha mbalimbali za Matukio katika afua hiyo



